Sheria na Masharti ya Ziada ya Google One
Mara ya Mwisho Kubadilishwa: 11 Novemba 2025 |Ili utumie Google One, ni sharti ukubali (1) Sheria na Masharti ya Google pamoja na (2) Sheria na Masharti haya ya Ziada ya Google One (“Masharti ya Ziada”). Masharti ambayo hayajafafanuliwa katika Masharti haya ya Ziada yamefafanuliwa katika Sheria na Masharti ya Google.
Tafadhali soma hati hizi kwa makini. Kwa pamoja, hati hizi zinajulikana kama “Masharti”. Zinabainisha unachoweza kutarajia kutoka kwetu unapotumia huduma zetu na tunachotarajia kutoka kwako.
Pia, tunakuhimiza usome Sera yetu ya Faragha ili uelewe vyema zaidi jinsi unavyoweza kusasisha, kudhibiti, kuhamisha na kufuta taarifa zako.
1. Huduma Yetu
Google One hutoa mipango ya usajili yenye nafasi ya hifadhi ya kulipia ambayo inatumiwa katika Gmail, huduma ya Picha kwenye Google na Hifadhi ya Google, ikijumuisha mipango ya usajili yenye manufaa ya ziada unayopewa na Google au kupitia washirika wengine. Google One pia hutoa mipango ya usajili na masalio ya AI kwa ufikiaji unaolipiwa wa vipengele fulani vya AI vilivyobuniwa na Google. Matumizi yako ya manufaa ya ziada ya Google au ya mshirika mwingine yanasimamiwa na sheria na masharti yanayotumika kwenye manufaa hayo. Huenda baadhi ya manufaa yasipatikane katika nchi zote na yanaweza kutegemea vizuizi vingine. Tafadhali tembelea Kituo cha Usaidizi cha Google One ili upate maelezo zaidi.
Huduma ya Google One inatolewa na asasi ya Google iliyobainishwa katika Sheria na Masharti ya Google. Unaponunua usajili wa Google One au masalio ya AI, unaingia katika mkataba tofauti na muuzaji, anayeweza kuwa asasi ya Google (angalia Kifungu cha 2) au mshirika mwingine. Iwapo una usajili wa Google One kupitia mshirika mwingine, basi usajili wako unaweza kusimamiwa na masharti ya ziada ya mshirika huyo.
Masalio ya AI
Unaweza kutumia masalio ya AI kuwezesha na kuchakata maombi yako kwenye vipengele vya AI vilivyobainishwa. Tutakufahamisha kuhusu idadi ya salio inayohitajika katika kitendo mahususi (k.m., kutayarisha video) kwenye bidhaa au kipengele husika. Google inahifadhi haki ya kubadilisha gharama ya salio ya kutumia vipengele vya AI. Masalio ya AI yanaweza tu kutumiwa kufikia vipengele fulani vya AI ambavyo huenda vinatolewa na Google mara kwa mara.
Muda wa kutumia masalio ya AI unaweza kuisha baada ya kipindi fulani, kama ilivyobainishwa ulipoyanunua.
Huna haki au umiliki katika masalio ya AI isipokuwa jinsi ilivyobainishwa kwenye Masharti haya. Huruhusiwi kuuza wala kuhamisha masalio ya AI kwa mtumiaji au akaunti nyingine au kujaribu kuuza au kuhamisha masalio ya AI. Unaponunua masalio ya AI, unalipia kabla ya kutumia vipengele fulani vya AI vilivyobainishwa. Masalio ya AI si sarafu, amana, bidhaa dijitali au aina yoyote ya njia ya kulipa na huwezi kuyabadilisha ili upokee malipo ya pesa. Masalio ya AI hutumiwa tu katika vipengele mahususi vya AI kwenye mfumo wa Google. Masalio yoyote ya AI ambayo hayajatumiwa yanaweza kupotea baada ya kusimamishwa au kukatishwa kwa mpango wako wa Google One, kwa mujibu wa sera zozote zinazotumika za kurejesha pesa.
Pata maelezo zaidi kuhusu masalio ya AI hapa.
2. Ununuzi na Malipo
Usajili wa Google One utatumika katika kipindi kisicho na kikomo na utatozwa mwanzoni mwa kila kipindi cha kutozwa, kulingana na masharti ya usajili wako (kwa mfano, kila wiki, kila mwaka au kipindi kingine), isipokuwa ujiondoe.
Unaponunua usajili wa Google One au masalio ya AI, ununuzi wako utasimamiwa na sheria na masharti tofauti na ya muuzaji. Kwa mfano, unapojisajili kwenye Google One au kununua masalio ya AI kupitia Duka la Google Play, ununuzi wako utasimamiwa na Sheria na Masharti ya Google Play.
Muuzaji wa usajili wa Google One au Masalio ya AI unayonunua kupitia Duka la Google Play ni:
- Kwa watumiaji walioko Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika: Google Commerce Limited
- Kwa watumiaji walioko nchini India: Google Ireland Limited
- Kwa watumiaji walio katika maeneo mengine ya Asia, Pasifiki: Google Digital Inc.
- Kwa watumiaji walioko nchini Marekani na kwingine duniani: Google LLC.
Unaponunua usajili wa Google One au masalio ya AI kupitia mshirika mwingine, mshirika huyo atatoza njia yako ya kulipa na atawajibika kutatua matatizo yoyote kuhusu malipo yako, ikiwa ni pamoja na ukatishaji na urejeshaji wa pesa.
Muuzaji akishindwa kukutoza bei ya usajili wa Google One, huenda usiweze kufikia Google One hadi utakaposasisha njia yako ya kulipa uliyompa muuzaji huyo. Ukikosa kusasisha njia yako ya kulipa ndani ya muda ufaao baada ya kupokea ilani, tunaweza kukatisha au kusimamisha idhini yako ya kufikia Google One.
3. Bei na Ofa
Ofa. Mara kwa mara, tunaweza kutoa vipindi vya kujaribu usajili wa Google One bila kulipia. Ukinunua usajili wa Google One unaojumuisha kipindi cha kujaribu, utapata idhini ya kufikia Google One katika kipindi cha kujaribu. Mwishoni mwa kipindi cha kujaribu na kwa kiwango kinachoruhusiwa na sheria inayotumika, utatozwa kiotomatiki bei ya usajili katika kila kipindi cha bili ikiwa ulimpa muuzaji njia sahihi ya kulipa na utaendelea kutozwa hadi utakapokatisha usajili wako. Ili uepuke kutozwa gharama zozote, ni lazima ukatishe usajili wako kutoka kwa muuzaji kabla ya mwisho wa kipindi cha kujaribu. Mara kwa mara, tunaweza pia kutoa mapunguzo katika usajili kwenye Google One. Sheria na masharti ya ziada, yakijumuisha masharti ya kujiunga, yanaweza kutumika kwenye ofa hizi na unaweza kusimamiwa na sheria na masharti yoyote ya ziada kama hayo kabla ya kutumia au kununua. Ofa hazitatumika panapopigwa marufuku au kuzuiwa na sheria inayotumika.
Mabadiliko ya bei. Mara kwa mara, tunaweza kubadilisha bei za usajili wa Google One au za masalio ya AI, kwa mfano, ili kuonyesha mfumuko wa bei, mabadiliko katika kodi zinazotumika, matoleo ya ofa, Google One au kwenye mahitaji ya biashara. Katika mabadiliko ya bei za usajili wa Google One, mabadiliko haya yatatekelezwa baada ya kipindi chako cha sasa cha kulipa kukamilika na unapodaiwa malipo yanayofuata baada ya kupokea ilani. Tutakupea ilani ya awali ya angalau siku 30 kuhusu kuongezeka kwa bei kabla ya kukutoza. Ukipewa ilani ya awali ya chini ya siku 30, mabadiliko hayatatekelezwa hadi baada ya malipo yanayofuata kudaiwa. Iwapo hungependa kuendelea kutumia usajili wako wa Google One kwa bei mpya, unaweza kuukatisha kama ilivyofafanuliwa katika sehemu ya Kukatisha kwenye Masharti haya na hutatozwa ada zaidi za usajili, mradi umetuarifu kabla ya mwisho wa kipindi cha sasa cha bili. Katika hali ambayo bei imeongezwa na unahitajika kutoa idhini, usajili wako utakatishwa isipokuwa ukikubali bei mpya.
4. Ukatishaji na Urejeshaji wa pesa
Ukatishaji na kujiondoa. Ukikatisha usajili wako, utaendelea kutumia Google One kwa muda uliosalia wa kipindi chako cha bili cha sasa, isipokuwa uwe na haki ya kukatisha papo hapo au haki nyingine za kukatisha au kujiondoa kama ilivyofafanuliwa zaidi katika Kituo cha Usaidizi. Ikiwa una haki ya kujiondoa na ungependa kufanya hivyo, ni lazima uwasilishe uamuzi wako wa kujiondoa kupitia taarifa dhahiri kwa muuzaji uliyenunua kwake. Ukiomba kuanzisha utekelezaji wa huduma katika kipindi cha kujiondoa, huenda ukahitajika kulipa kiasi kilichorekebishwa kulingana na huduma ulizopokea hadi utakapowasiliana na muuzaji kuhusu kujiondoa kwenye mkataba.
Ukichagua kufuta Google One kupitia ufutaji wa huduma, unakubali kwamba unaweza kupoteza idhini ya kufikia huduma za Google One papo hapo. Ikiwa ungependa kuendelea kutumia huduma za Google One katika kipindi kilichosalia cha bili, tafadhali katisha usajili wako badala ya kufuta Google One.
Kurejesha pesa. Ikiwa ulinunua usajili wa Google One au masalio ya AI, sera ya kurejesha pesa itatumika. Utahitaji kuwasiliana na muuzaji uliyenunua kwake ili uombe kurejeshewa pesa. Unaweza kuwa na haki za mtumiaji kwa mujibu wa sheria inayotumika ambayo haiwezi kudhibitiwa na mkataba. Masharti haya hayadhibiti haki hizo.
5. Huduma kwa Wateja
Google One inaweza kujumuisha idhini ya kufikia huduma kwa wateja kwenye huduma fulani za Google. Ikitokea kuwa timu ya huduma kwa wateja imeshindwa kushughulikia ombi lako, tunaweza kukuelekeza kwa timu ya huduma kwa wateja ya huduma husika ya Google. Usajili wako wa Google One ukikatishwa au kusimamishwa, matatizo ambayo hayajashughulikiwa na timu ya huduma kwa wateja yanaweza pia kusimamishwa na huenda ukahitaji kutuma ombi jipya baada ya kurejeshewa usajili wako. Tafadhali tembelea Kituo chetu cha Usaidizi ili upate maelezo zaidi kuhusu huduma kwa wateja.
6. Kutumia Pamoja na Familia
Unaweza kutumia na kikundi cha familia yako manufaa fulani ya usajili wako wa Google One (“Kutumia Pamoja na Familia”). Ikiwa hutaki kutumia manufaa yoyote na kikundi cha familia yako, ni sharti uzime kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia kwenye Google One au uondoke katika kikundi cha familia yako. Wasimamizi wa mipango ya Google One pekee ndio wanaweza kuongeza wanafamilia na kuwasha au kuzima kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia katika usajili wa Google One. Tafadhali tembelea Kituo chetu cha Usaidizi ili upate maelezo zaidi kuhusu kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia.
Ikiwa wewe ni mwanakikundi wa familia kwenye Google One, wanakikundi wa familia yako wataweza kuona taarifa fulani kukuhusu. Kwa mfano, ukijiunga na kikundi cha familia ambapo kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia cha Google One kimewashwa, wanakikundi (na walioalikwa) wa familia wanaweza kuona jina, picha, anwani ya barua pepe, vifaa ambavyo umehifadhi nakala ya data, masalio ya AI uliyotumia pamoja na nafasi ya hifadhi unayotumia. Wanakikundi wa familia wanaweza pia kuona iwapo mwanafamilia ametumia manufaa fulani ya ziada yaliyojumuishwa katika usajili wa Google One.
Ikiwa wewe ndiwe msimamizi wa mpango wa Google One katika kikundi cha familia yako na uzime kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia au uondoke kwenye kikundi cha familia, wanakikundi wengine wa familia yako hawataweza kutumia usajili wa Google One. Ikiwa msimamizi wako wa mpango wa Google One amekupa idhini ya kutumia Google One kupitia kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia, hutaweza kutumia Google One ukiondoka kwenye kikundi cha familia yako au msimamizi wako wa mpango wa Google One akizima kipengele cha Kutumia Pamoja na Familia au akiondoka katika kikundi cha familia.
7. Kuhifadhi na Kurejesha Nakala za Data Kwenye Simu
Google One inaweza kujumuisha kipengele kilichoboreshwa cha kuhifadhi na kurejesha nakala za data (“Kuhifadhi na Kurejesha Nakala”) katika vifaa vya mkononi vinavyotimiza masharti. Huenda ukahitaji kuweka kwenye kifaa na kutumia programu za ziada, kama vile programu ya Picha kwenye Google ili utumie kipengele cha Kuhifadhi na Kurejesha Nakala. Unaweza kubadilisha chaguo zako za Kuhifadhi na Kurejesha Nakala wakati wowote katika programu ya Google One. Usajili wako wa Google One ukisimamishwa au ukikatishwa, unaweza kupoteza idhini ya kufikia data iliyohifadhiwa katika kipengele cha Kuhifadhi na Kurejesha Nakala baada ya kipindi fulani, kwa mujibu wa sera zinazotumika za huduma ya 'Hifadhi ya Nakala kwenye Android'.